Tanzania
imeutaka Umoja wa Mataifa UN kufanya uchunguzi wa kina na huru kuhusu chanzo
cha tukio la shambulio la waasi wa kundi la ADF lililosababisha vifo vya
wanajeshi 14 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania JWTZ waliokuwa
wakilinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,DRC.
Akizungumza
kwenye shughuli ya kuaga miili ya wanajeshi hao iliyofanyika katika viwanja vya
makao makuu ya JWTZ Upanga,Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kasim
Majaliwa amesema Umoja wa Mataifa unapaswa kuchunguza tukio hilo na kwamba
serikali ya Tanzania inaamini uchunguzi huo utaanza hivi karibuni
"Japo
matukio kama haya hutegemewa na hutokea,lakini hatujawahi kupoteza wapiganaji
wengi na kwa mpigo kama hivi”.Amesema Waziri Mkuu Majaliwa
Hata
hivyo Waziri Mkuu Majaliwa amewataka wanajeshi wa Tanzania wanaolinda amani
nchini DRC wasirudi nyuma au kukatishwa na tukio hilo badala yake amewaasa kuchukua
tahadhari zaidi.
Akizungumza
kwenye shughuli hiyo,Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk. Hussein Mwinyi
amesema wanajeshi waliouawa ni mashujaa wa Taifa na kuondoka kwao kumeacha
pengo kubwa katika Taifa.
Dkt. Mwinyi amesema “Kuondoka kwa wanajeshi hawa kusiturudishe nyuma
katika majukumu yetu ya kazi bali iwe chachu ya utendaji kazi na kutoogopa chochote
kilichopo mbele yetu”
Naye Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo amesema mbali na wanajeshi 14 waliouawa,kuna mwanajeshi mmoja hajulikani alipo na kwamba wanajeshi wengine 44 ambao ni majeruhi wa tukio hilo wanaendelea na matibabu katika miji ya Kampala, Kinshasa na Goma.
Naye Mkuu wa Majeshi Jenerali Venance Mabeyo amesema mbali na wanajeshi 14 waliouawa,kuna mwanajeshi mmoja hajulikani alipo na kwamba wanajeshi wengine 44 ambao ni majeruhi wa tukio hilo wanaendelea na matibabu katika miji ya Kampala, Kinshasa na Goma.
Viongozi
wengine waliohudhuria shughuli hiyo ni Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete,Katibu
Mkuu wa zamani wa Umoja wa Afrika Dkt Salim Ahmed Salim,Katibu Mkuu wa Jumuiya
ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC Dkt. Stagomena Tax,Mwakilishi wa
Umoja wa Mataifa UN na viongozi wa vyama vya siasa,dini na taasisi mbalimbali