Lehemu au maararufu kama cholesterol kwa Kiingereza ni aina ya fati kama nta (wax), ambayo huwa kwenye damu ikizunguka sehemu mbalimbali mwilini. Ni sehemu muhimu sana ya kuta za seli za mwili, homoni za mfumo wa uzazi, Vitamini D na kuta za mishipa ya fahamu.
Je, kuna aina ngapi za lehemu?
Lehemu hupatikana kwenye damu kama lipoproteins (muunganiko wa lehemu na protini). Lipoproteins muhimu ni;
- Very Low Density Lipoprotieins (VLDL)
- Low density Lipoproteins(LDL) na
- High Density Lipoproteins (HDL).
VLDL na LDL hubeba lehemu kutoka kwenye ini na kuipeleka kwenye seli mbalimbali kwa ajili ya kazi za mwili. HDL huondoa lehemu ambayo haijatumika au imezidi kwenye seli za mwili na kuirudisha kwenye ini ili ivunjwevunjwe na kutolewa kama uchafu.
Lehemu Yenye Athari Mbaya kwa Afya.
Kama tulivyoona kuna aina tofauti za lehemu kwenye damu, sio zote zina athari mbaya kwa afya. LDL (Low Density Lipoprotein) ni lehemu mbaya pale inapozidi kwenye damu. HDL (High Density Lipoprotein) huwa haina madhara mabaya pale inapozidi kwenye damu, ila ikipungua zaidi ya kawaida na LDL kuongezeka huleta hatari kwa afya.
Vyanzo Vya Lehemu
Kwa kawaida mwili hupata lehemu kutoka kwenye;
- Ini ambalo hutengeneza karibu asilimia 75 ya lehemu yote mwilini.
- Vyakula mbalimbali vya mafuta ambavyo huchangia asilimia 25 ya lehemu.
Vitu vinavyosababiisha mwili kutengeneza lehemu nyingi zaidi ya kawaida.
Lehemu hatari zaidi ni ile inayotengenezwa na ini kuliko ile inayopatikana kwenye chakula. Magonjwa ya kurithi ya utengenezaji wa lehemu na tabia za ulaji vyakula huchangia ini kutengeneza lehemu nyingi zaidi ya kawaida. Ulaji wa vyakula vya fati ambazo ni saturated na trans saturated huongeza kasi ya ini kutengeneza lehemu. Pia kutofanya mazoezi na uvutaji sigara huchangia lehemu kuongezeka.
Vyakula Vinavyoongeza Lehemu Mwilini
Saturated fats hupatikana hasa kutokana na vyakula vya wanyama kama nyama nyekundu, maziwa (whole milk), siagi, hotdogsna transaturated fats hupatikana kwenye margarines (kama blueband, kimbo na mafuta mengine ya kuganda), chipsi za kukaanga, keki, biskuti, vyakula vya kukaangwa kwenye makopo.
Unsaturated fats zinapatikana zaidi kwenye mafuta ya mimea kama pamba, alizeti, zeituni (Olive), karanga, mawese, soya, canola,mahindi na maparachichi. Pia samaki wana unsaturated fats aina ya omega-3 na omega-6. Aina hizi za fati husaidia kuongeza HDL kwenye damu ambayo huondoa lehemu inayozidi kwenye seli na mishipa ya damu, hivyo ni vizuri kutumia mafuta ya mimea katika chakula kuliko ya wanyama.
Lehemu ina uhusiano gani na ugonjwa wa moyo?
LDL inapozidi kwenye damu huachia lehemu ambayo huenda kujikusanya ndani ya mishipa ya damu na ya moyo polepole kitendo kiitwacho atherosclerosis. Hali hii huweza kusababisha mishipa ya damu ya moyo kuziba na hivyo kutokea heart attack kutokana na baadhi ya misuli ya moyo kukosa damu na moyo kushindwa kufanya kazi vizuri.
Lehemu ina uhusiano gani na shinikizo la damu la kupanda (hypertension) na kiharusi (stroke)?
Hali hii ya kujaa kwa lehemu kwenye mishipa ya damu hupunguza ukubwa wa tundu la mishipa ya damu, na hivyo kusababisha damu kupita kwa presha kubwa zaidi. Hali hii huendelea na kusababisha presha ya damu kuongezeka mwili mzima na hivyo kuwa shinikizo la damu la kupanda (hypertension).
Kwenye mishipa ya damu inayoingia kwenye ubongo, lehemu ikijaa huweza kuziba mishipa hiyo au kuchangia ipasuke na hivyo kusababisha kiharusi (stroke).
Nifanye nini kujua kama kiwangi cha lehemu yangu kwenye damu ni cha kawaida?
Ili kuweza kujua kiwango cha lehemu kwenye damu yako, kipimo cha Lipid (lipoprotein) Profile hufanyika hospitalini. Hiki hupima aina za fati kwenye damu yako ikijumuisha kiasi chote cha cholesterol, LDL,HDL na triglycerides (aina nyingine ya fati).
Njia za kupunguza lehemu mwilini.
Lehemu inapozidi kwenye damu inaongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo, shinikizo la damu la kupanda na kiharusi, hivyo ni muhimu kupunguza kiwango cha lehemu kwenye damu. Kuna njia zifuatazo;
- Kufanya mazoezi
- Kupunguza vyakula vyenye fati
- Kula matunda, mboga za majani na nafaka zisizokobolewa zaidi kwenye mlo wako.
- Kupunguza uzito kama mtu ana uzito mkubwa.
- Kuacha kuvuta sigara
- Kupunguza unywaji wa pombe.
- Kutumia dawa za kupunguza lehemu, dawa hizi huitwa statins. Dawa hizi hutolewa kwa maelekezo ya daktari.